Mholanzi kuongoza jopo la uchunguzi Sudan Kusini

23 Agosti 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemteua Meja Jenerali Patrick Cammaert kutoka Uholanzi kuongoza jopo huru maalum litakalochunguza ghasia zilizotokea Juba Sudan Kusini mwezi Julai mwaka huu na hatua zilizochukuliwa na ujumbe wa umoja huo UNMISS.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema uchunguzi huo utatathmini ripoti za matukio ya mashambulizi ya raia na visa vya ubakaji vilivyotokea ndani au karibu na kituo cha ulinzi wa raia huko Juba.

Halikadhalika itabaini hatua za UNMISS na iwapo zilikuwa sahihi katika kuhakikisha wanazuia vitendo hivyo dhidi ya raia kwenye kituo hicho na mazingira ya shambulio lingine kwenye hoteli ya Terrain.

Jopo hilo litakwenda Juba kuhoji baadhi ya watu na ripoti inatarajiwa kukabidhiwa Katibu Mkuu ndani ya mwezi mmoja ambapo matokeo yatawekwa hadharani.

Meja Jenerali mstaafu  Cammaert hivi karibuni aliongoza bodi ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kwenye mapigano yaliyofanyika huko Malakal, Sudan Kusini mwezi Februari mwaka huu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter