Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Silaha za maangamizi ni hatari lakini mjadala unakwama- Ban

Silaha za maangamizi ni hatari lakini mjadala unakwama- Ban

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu udhibiti wa ueneaji wa silaha za maangamizi ikiwemo zile za nyuklia na kibaiolojia.

Akizungumza kwenye mjadala huo ulioandaliwa na Malaysia ambayo inashikilia urais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Agosti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema suala hilo ni jambo ambalo jamii ya kimataifa inawajibika.

Hata hivyo amesema wakati dunia inakabiliwa na kitisho kikubwa kutokana na silaha hizo, bado ajenda hiyo imekumbwa na mkwamo katika maeneo mengi, akigusia mvutano wakati wa mkutano wa tathmini mkataba wa udhibiti wa kuenea nyuklia, NPT.

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa nchi kujikita katika ukweli halisi ya kwamba njia pekee ya kuzuia utokomezaji wa binadamu, mazingira na athari nyingine ambazo silaha hizo zinaweza kusababisha ni kwa kuachana nazo kabisa.

Na kwa baraza la usalama amesema…

“Natoa wito pia kwa baraza hili kuzingatia jinsi ya kuimarisha azimio namba 1540 kuhakikisha vikundi visivyo vya kiserikali havipati silaha hizi hatari.”