Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yachukua hatua kukidhi mahitaji ya kiafya Nigeria

WHO yachukua hatua kukidhi mahitaji ya kiafya Nigeria

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limechukua hatua za dharura kukidhi mahitaji ya afya kwenye eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria ambako vikundi vya waasi vimekuwa vikisambaratisha huduma za afya.

Hatua hizo ni pamoja na kuwasili kwa jopo la dharura la afya huko Maiduguri kutathmini mahitaji ya afya kwa watu zaidi ya Laki Nane kwenye eneo ambalo awali lilikuwa linashikiliwa na vikundi vilivyojihami.

Katika jimbo la Borno, nusu ya vituo vya afya havifanyi kazi, kiwango cha utapiamlo kinakadiriwa kuwa asilimia 14 wakati huu ambapo visa viwili pia vya Polio viliripotiwa katika eneo hilo wiki iliyopita.

WHO katika taarifa yake inasema tathmini inaonyesha kuwa mgonjwa mmoja wa Polio kati ya hao wawili yuko katika eneo ambalo bado haliwezi kufikiwa huku Surua nayo ikiwa imeripotiwa kwenye eneo hilo.