Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Najutia nilichofanyia Timbuktu- Al Mahdi

Najutia nilichofanyia Timbuktu- Al Mahdi

Mshtakiwa katika kesi ya uhalifu wa kivita dhidi ya eneo la Timbuktu huko Mali, Ahmad Al Faqi Al Mahdi amesema anajutia sana kitendo chake cha kuhusikana  uharibifu wa maeneo ya kihistoria na kidini kwenye mji huo, ikiwemo makavazi.

Mahdi amesema hayo katika taarifa aliyosoma kwa lugha ya kiarabu na kufasiriwa kwa kiingereza mbele ya majaji wanaoendesha kesi yake katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, huko The Hague, Uholanzi.

 “Kwa majuto makubwa na kwa machungu makubwa, imenibidi kukubali makosa, na mashtaka yote dhidi yangu ni sawa na sahihi.”

Akaenda mbali zaidi

“Nimekosa sana.  Nina majuto makubwa. Najutia mno athari zote mbaya ambazo vitendo vyangu vimesababisha. Najutia kile nilichofanyia familia yangu Timbuktu na taifa langu la Mali na najutia sana kile nilichofanyia jamii yote ya kimataifa.”

Na hatimaye akatoa ahadi..

“Napenda niwapatie ahadi ya dhati kuwa hili lilikuwa ni kosa langu la kwanza na la mwisho kuwahi kutenda”.

Baada ya pande zote kusikilizwa, majaji watatu katika kesi hiyo ya kwanza kabisa dhidi ya Mali na pia kuangazia mali za turathi ikiwemo makavazi, wataamua iwapo mshtakiwa amepatikana na hatia au la.