Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wawakumbuka wafanyakazi wake waliopoteza maisha Iraq miaka 13 iliyopita:

UM wawakumbuka wafanyakazi wake waliopoteza maisha Iraq miaka 13 iliyopita:

Hafla maalumu ya kumbukumbu imefanyika leo Ijumaa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuwaenzi wafanyakazi wake waliopoteza maisha miaka 13 iliyopita baada ya hotel ya Canal kushambuliwa kwa bomu mjini Baghdad nchini Iraq.

Tarehe 19 Agosti mwaka 2013 , mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Sergio Vieira de Mello aliuawa pamoja na wafanyakazi wengine 22 na mamia ya  wengine kujeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema alikuwa akifanya kazi kama balozi wa Sweden mjini Washington wakati taarifa za shambulio hilo zilipotangazwa.

(SAUTI YA ELIASSON)

"Wale walioshambulia Umoja wa Mataifa walitaka kututisha, tujihisi dhoofu na kukata tamaa. Tunaowaenzi leo wanatuhamasisha kuwa imara na kujikita katika kusonga mbele. Hii ni changamoto tunayokumbana nayo kila mahali duniani hivi leo, kuanzia Syria hadi Sudan Kusini, kuanzia Yemen hadi Libya, kutoka Somalia hadi Afghanistan, ambako wafanyakazi wa usaidizi wa kibinadamu na walinda amani wamepoteza au wanahatarisha maisha yao”

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Usaidizi wa Kibinadamu ambapo Umoja wa Mataifa unawaenzi wafanyakazi wa misaada kote ulimwenguni ambao wanapitia hatari kila siku kusaidia wengine.