Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumzia uamuzi wa mahakama Marekani kuhusu Kipindupindu Haiti

Ban azungumzia uamuzi wa mahakama Marekani kuhusu Kipindupindu Haiti

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametambua uamuzi wa mahakama ya rufaa nchini Marekani kupitisha uamuzi unaounga mkono kipengele kinachozuia umoja huo kufikishwa mahakama kwa mujibu wa mkataba uliouanzisha.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa jana kwenye rufaa ya kesi ya George na wenzake dhidi ya Umoja wa Mataifa na washirika juu ya sakata la kipindupindu huko Haiti.

Kupitia msemaji wake, Ban amesema anajutia sana machungu waliyopata wananchi wa Haiti kutokana na mlipuko wa kipindupindu na kwamba umoja huo una wajibu wa kimaadili kwa wahanga wa ugonjwa huo na kusaidia Haiti katika kukabiliana na athari za mlipuko huo.

Amesema Umoja wa Mataifa unatoa usaidizi huo kupitia ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama na mifuko bora ya afya.

Jitihada za kitaifa na kimataifa zimesaidia kupunguza visa vya kipindupindu kwa asilimia 90 tangu mlipuko ufikie kiwango cha juu mwaka 2011.

Hata hivyo Ban amesema kutokomeza kipindupindu Haiti kunahitaji azma ya serikali na jamii ya kimataifa na zaidi ya yote kupata rasilimali zinazohitajika ili kutekeleza wajibu wa pamoja.