Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia za uchunguzi wa afya zinaibua matatizo zaidi, tuwe makini- IARC

Teknolojia za uchunguzi wa afya zinaibua matatizo zaidi, tuwe makini- IARC

Ongezeko la teknolojia za kisasa za kubaini matatizo ya kiafya mwilini, limesababisha pia athari mbaya za kiafya kwa kuwa watu wanatibu hata uvimbe ambao hauwezi kuwa na madhara kiafya.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na taasisi ya saratani inayofanya kazi na shirika la afya duniani, WHO, IARC, ripoti inayoangazia jinsi uwepo wa vifaa vya kisasa unachochea watu kuchunguza koromeo au dundumio.

Taasisi hiyo ilishirikiana na taasisi ya kitaifa ya saratani Italia, Aviano ambapo imetaja mashine kama vile CT-Scan, MRI na Ultrasonography kuwa zinaibua hata uvimbe ambao hauna madhara lakini watu wanachukua hatua, mathalani tezi dundumio ambayo imeripotiwa zaidi Korea Kusini.

Mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo Dokta Silvia Franceschi amesema idadi kubwa ya wagonjwa wanaobainika kuwa na saratani ya koromeo wanapatiwa tiba ya kukatwa kabisa koromeo au tiba hatari kama vile mionzi bila uthibitisho kuwa wakifanyiwa tiba hiyo wataendelea kuishi.

Kwa mantiki hiyo, ripoti hiyo inataka watu kuwa makini kabla ya kuamua kufanya uchunguzi wa tezi dundumio.