Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa nishati ya jua waleta nuru kwa wakazi wa Kidal, Mali

Mradi wa nishati ya jua waleta nuru kwa wakazi wa Kidal, Mali

Nchini Mali, mradi wa kuzaliwasha umeme kwa kutumia nishati ya jua umeleta ahueni kwa wakazi wa mkoa wa Kidal, kaskazini mwa Mali, ambako ukosefu wa usalama ulikwamisha upatikanaji wa huduma ya umeme.

Mradi huo unaofadhiliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA kwa ushirikiano na Canada umepatia umeme kaya zaidi ya 1,500 ambapo sasa watoto wanaweza kusoma hata nyakati za usiku na wanawake nao kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii bila hofu ya ukosefu wa usalama.

Mmoja wa wanufaika ni Aicha Abdoulaye.

(Sauti ya Aicha)

Tunatumia kuchaji simu zetu za kiganjani. Kabla ya hapo ilikuwa vigumu kuchaji simu. Sasa hivi usiku kuna mwanga tunaweza kuona kile tunachofanya hadi tunapokwenda kulala na watoto wetu wanaweza kusoma.”

Mradi huo umegharimu dola za kimarekani 150,000 ambapo kaya husika zimepatiwa betri ya kuhifadhi umeme huo inayopata chaji kutokana na jua.