Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Milioni 50 kutoka CERF kusaidia dharura zilizosahaulika

Dola Milioni 50 kutoka CERF kusaidia dharura zilizosahaulika

Hii leo Stephen O’Brien ambaye ni mratibu wa masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa, OCHA, ameidhinisha dola millioni 50 kutoka kwa mfuko wa dharura wa umoja huo, CERF ili  kusaidia operesheni sita za usaidizi wa kibinadamu zilizosahaulika.

Taarifa ya OCHA imesema fedha hizo zitasaidia mahitaji ya kibinadamu ya takribani watu milioni mbili ikiwemo wakimbizi Laki Mbili, wakimbizi wa ndani mia sita sitini na tano elfu na wenyeji wenyeji mia tano na thelathini elfu wanaohifadhi wakimbizi.

Akizungumzia hatua hiyo, O’Brien amesema fedha hizo zitaokoa maisha ya wahitaji wengi walio kwenye majanga yaliyosahaulika.

Fedha nyingine zaidi dola milioni 35 zitawezesha wadau wa kibinadamu kushughulikia dharura nyingine za misaada Afrika ambazo zinatokana na sababu kadhaa kama vile migogoro ya kivita , kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Baadhi ya nchi nufaika ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR,  itapata dola million Tisa,  Chad dola milioni 10, DRCongo dola millioni 11 na dola milioni Tano zitapelekwa Rwanda ili kusaidia wakimbizi kutoka Burundi na DR Congo.

Bwana O’Brien amehimiza mataifa yanayojiweza, mashirika ya kikanda na watu binafsi kuongezea usaidizi wao kusaidia maisha ya binadamu akieleza kuwa mfuko wa CERF unakumbwa na ukata.