Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya utu wa kibinadamu Ban apigia chepuo kampeni ya #World You’d Rather

Siku ya utu wa kibinadamu Ban apigia chepuo kampeni ya #World You’d Rather

Watu Milioni 130, idadi ambayo ni kubwa zaidi kufikiwa, hivi sasa wanaish kwa kutegemea misaada ya kibinadamu.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu inayoadhimishwa leo.

Ban amesema watu hao ambao wameenea sehemu mbali mbali duniani, wakiwekwa pamoja wataunda taifa ambalo litakuwa ni la 10 kwa kuwa na idadi kubwa ya watu.

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon akiwa na mmoja wa watoto wakimbizi wa ndani alipotembelea Juba, Sudan Kusini. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Hata hivyo amesema licha ya kwamba takwimu hizo zinastusha, bado hazitoi picha halisi ya machungu yanayokumba watu hao ambao amesema hawana tofauti na watu wengine, lakini watu hao wanalazimika kuchagua kati ya kununua chakula au dawa kwa watoto wao, watoto ambao wanapaswa pia kuchagua kati ya kwenda shule au kusaidia familia zao, familia ambazo amesema ziko hatarini kushambuliwa kwenye makazi yao au kufanya safari hatari baharini.
image
Boya la uokozi na baadhi ya vifaa vya wahamiaji ambao vimekubwa baharini. (Picha:UN /UNHCR/Phil Behan)
Ban amesema suluhu ya janga hilo si rahisi wala haliwezi kupatikana haraka, bali ni mambo ambavyo kila mmoja anapaswa kufanya leo na kila siku ikiwemo kuonyesha upendo, kupaza sauti dhidi ya ukiukwaji wa haki na kufanya kazi kuleta mabadiliko.
image
Utachagua lipi kati ya hayo? kunywa maji yenye vijidudu vya kipindupindu au kuvuka eneo lenye mabomu yaliyotegwa ardhini kuteka maji safi na salama? Hayo ndiyo maisha ya waliofurushwa makwao. (Picha:WHD-Screenshot)
Hivyo Katibu Mkuu amesema katika siku hii ya leo ambayo inatumika pia kuenzi watoa usaidizi wa kibinadamu ametoa wito watu kusaini kampeni ya Umoja wa Mataifa iitwayo World You’d Rather  ambayo amesema pamoja na kulenga kupanua uelewa wa watu kuhusu mazingira ya wanaohitaji misaada ya kibinadamu, kampeni ina lengo la msingi, kuchangisha fedha kwa ajili ya mfuko wa dharura ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, CERF, kusajili watu kila mahali kama wajumbe wa amani.

Ban amesema viongozi waliahidi kuhakikisha kila mtu anajumuishwa ili asichwe nyuma katika maendeleo endelevu, hivyo kwa siku ya leo suala hilo lipatiwe kipaumbele kama njia ya kutimiza SDGs na zaidi ya hayo..

(Sauti ya Ban)

“Katika siku hii ya utu wa kibinadamu, nawasihi muwakumbushe viongozi watimize ahadi. Wazue na kumaliza mizozo. Wazingatie maadili ya kimataifa. Waondokane na kusaka kutoa misaada na badala yake kuweka mazingira ya watu kutosheka. Hebu na tutambue kuwa sisi sote ni binadamu na tunawajibika pamoja.”