Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya wajawazito na watoto tatizo linaloendelea: WHO

Vifo vya wajawazito na watoto tatizo linaloendelea: WHO

Tuanze na masuala ya afya, Shirika  la afya ulimwenguni WHO,  linasema vifo vya  akina mama wakati wa ujauzito, kujifungua, vifo vya watoto wachanga katika siku 28 za mwanzo, na watoto wasio riziki  ni kubwa kuliko inavyoripotiwa. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Kwa mujibu wa WHO,  kote duniani zaidi ya wanawake laki tatu hufa wakati wa ujauzito na kujifungua, zaidi ya watotomilioni mbili hufa katika siku 28 za mwanzo huku wengine zaidi ya milioni mbili wakiwa ni watoto wasio riziki.

Hata hivyo shirika hilo la afya ulimwenguni limesisitiza kuwa vifo vingi vya watoto wachanga na wale wanaozaliwa wakiwa wamekufa vinazuilika kwa kuwa na huduma bora za afya wakati wa ujauzito na kujifungua na kuongeza kuwa karibu vifo vyote vya watoto wasio riziki na nusu ya wachanga havisajiliwi.

Ian Askew ni Mkurugenzi kitengo cha afya ya uzazi na utafiti katika WHO.

(SAUTI IAN)

‘‘Idadi hii ni makadirio, na tatizo la pili tunalokabiliana nalo ni kwamba kwa kuwa hakuna kumbukumbu za vifo na vizazi vya watoto, ni vigumu sana kufahamu sababu za vifo’’