Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni kubwa ya chanjo kuwahi kufanywa na WHO kuanza DRC na Angola

Kampeni kubwa ya chanjo kuwahi kufanywa na WHO kuanza DRC na Angola

Moja ya kampeni kubwa kabisa ya chanjo ya dharura kuwahi kufanyika barani Afrika , itaanza nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Angola.

Kampeni hiyo itakayoanza wiki hii ni dhidi ya homa ya manjano , ikihusisha Shirika la Afya Duniani(WHO) na wadau wake, kwa lengo la kudhibiti mlipuko wa homa hiyo ambayo tayari imeshakatili maisha ya watu zaidi ya 400 na wengine kwa maelfu wanaugua.

Likishirikiana kwa karibu na wizara za afya za nchi zote mbili shirika la WHO linaratibu wadau wengine 56 , ili kuwachanja watu zaidi ya milioni 14, dhidi ya homa ya manjano katika maeneo zaidi ya 8000.

Kampeni ya dharura ya homa ya manjano imeshawafikia watu zaidi ya milioni 13 Angola na zaidi ya milioni 3 DRC.