Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waridhia jeshi la kikanda kupelekwa Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa waridhia jeshi la kikanda kupelekwa Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio kuidhinisha kikosi cha ulinzi cha kikanda kwa ajili ya Sudan Kusini.

Kikosi hicho kitakachokuwa na askari 4,000 kimeridhiwa baada ya azimio hilo kupigiwa kura na baraza hilo ambapo nchi 11 ziliunga mkono.

Kikosi hicho kitakuwa nchini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, makao makuu yakiwa mji mkuu, Juba na kitapatiwa mamlaka ya kutumia njia zote za lazima ili kutekeleza wajibu wake.

Azimio hilo namba 2304 la mwaka huu wa 2016 pamoja na kuongeza muda wa UNMISS hadi tarehe 15 Disemba mwaka huu, limesihi nchi wanachama wa ukanda huo kuharakatisha uchangiaji wanajeshi ili kikosi hicho kiweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo.

Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kwa upande wake inawasiliana na nchi za IGAD na muungano wa Afrika kuwezesha kupelekwa kwa kikosi hicho kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya IGAD iliyotolewa tarehe Tano Agosti baada ya kikao cha wakuu wa nchi hizo.