Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yachukua hatua kudhibiti ugonjwa unaokumba mifugo Ulaya

IAEA yachukua hatua kudhibiti ugonjwa unaokumba mifugo Ulaya

Wataalamu 36 wa mifugo kutoka nchi 22 barani Ulaya wanaanza kupatiwa mafunzo leo kwenye maabara kuhusu jinsi ya kubaini ugonjwa wa mifugo unaojulikana kama LSD unaoenea kwa kasi kubwa barani humo.

Mafunzo hayo katika maabara ya pamoja ya shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA na lile la chakula na kilimo, FAO utawezesha kubaini ugonjwa huo unaosababisha  ngozi kuwa na malengelenge na hatimaye ngozi kuharibika.

IAEA inasema tayari wamebaini ugonjwa huo nchini Ugiriki, Bulgaria, Macedonia, Serbia, Albania na Montenegro.

Virusi vya ugonjwa huo huambukizwa kupitia mgusano na mnyama aliyeambukizwa, vyakula vyenye virusi hivyo na kupitia nzi na chawa.

Ingawa ugonjwa huo hauna madhara yoyote kwa binadamu, IAEA inasema unaweza kuenea kwa wanyama na kusababisha hasara kubwa kiuchumi.