Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaonya kuhusu msongamano na uhaba wa ufadhili Sudan Kusini

UNHCR yaonya kuhusu msongamano na uhaba wa ufadhili Sudan Kusini

Shirika la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), limesema nchi jirani za Sudan Kusini zinahaha kukidhi mahitaji ya maelfu ya wakimbizi wanaoendelea kukimbi machafuko nchini mwao, huku kukiwa na ufadhili mdogo kwa operesheni za kuwasaidia.

Kwa mujibu wa UNHCR, tayari kuna wakimbizi 930,000 katika ukanda mzima, huku wengine wengi wakiwasili kila siku.

UNHCR imesema ina hofu kuwa wakati idadi ya wakimbizi ikizidi kuongezeka, fedha za kukidhi mahitaji ya msingi  zinadidimia, huku kukiwa na msongamano katika maeneo ya kuwapa hifadhi wakimbizi hao.

Uganda pekee imepokea wakimbizi wapya laki moja na kumi elfu, huku Sudan ikipokea wakimbizi wapya laki moja, nchi hizo mbili zikiwa zimepokea asilimia 90 ya wakimbizi wapya.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR, Geneva

 “Wakati kukiwa na mahitaji ya dharura kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa Sudan Kusini ambayo sasa ni 930,000, UNHCR inakabiliwa na uhaba wa ufadhili. Ni dola milioni 122 tu zimepokelewa, ikiwa ni asilimia 20 pekee ya dola milioni 608.8 zinazohitajika na UNHCR nchini Sudan Kusini na katika nchi sita zinazotoa hifadhi, kwa hiyo shughuli nyingi za zimesitishwa ili kutoa usaidizi muhimu zaidi wa kuokoa maisha kwa wakimbizi wanaowasili upya.”