Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tujenge madaraja badala ya kuta- Ban

Tujenge madaraja badala ya kuta- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ameshiriki katika hafla ya kushuhudia kurejea shuleni kwa watoto wakimbizi kutoka Syria na Guatemala, waliopata hifadhi huko California, Marekani.

Ban akizungumza nao amewaelezea uzoefu wake akisema hata yeye akiwa na umri wa miaka Sita, alifurushwa makwao na familia yake wakati wa vita vya Korea.

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa ulimpatia msaada na sasa anawakilisha taasisi hiyo, akiwapatia msaada wa vifaa vya shule ili warejee shuleni na hivyo kama yeye aliweza, basi hata wao wataweza kufanikiwa.

Kwa mantiki hiyo amewaambia wasikate tamaa, badala yake wawe na matumaini, wafanye kazi kwa bidii na kutangamana vyema na jamii hiyo ambayo imewakubali.

Amegeukia pia jamii ya kimataifa akiisihi iendelee kukirimu wakimbizi na wahamiaji, akipongeza zaidi jimbo la California kwa kufungua milango zaidi kwa kundi hilo.

Ban amesema kamwe jamii isiruhusu shinikizo la hofu na migawanyiko badala yake zikaribishe kwenye jamii zao marafiki na majirani na zijenge madaraja badala ya kuta.