Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD kusaidia mradi wa Mexico unaohusiana na maendeleo vijijini

IFAD kusaidia mradi wa Mexico unaohusiana na maendeleo vijijini

Shirika la kimataifa la ufadhili wa maendeleo ya kilimo IFAD, ambalo ni shirika la Umoja wa mataifa kwa ajili ya maendeleo vijijini, na serikali ya Mexico , wametia saini makubaliano ya kuchagiza ujasiriamali miongoni mwa watu masikini vijijini wanaopokea msaada wa huduma za kijamii.

Muafaka huo utashuhudia mradi wa ujumuishi vijijini ukitekelezwa katika manispaa 26 kwenye mikoa ya Guerrero, Hidalgo na Zacatecas na kuzifaidi familia 12,800.

Jumla ya gharama zote za mradi ni dola 19.5 , na kati ya fedha hizo IFAD itafadhili dola milioni 7.1.

Fedha zingine zitakazosalia zitafadhiliwa na serikali ya Mexico na watu watakaofaidika na mradi huo. Mbali ya kuwasaidia watu kuishi maisha ya hadhi kwa kupokea msaada wa fedha taslim, pia IFAD inasema utasaidia kubadili maisha ya watu wengi masikini vijijini ambao kwa sasa wanategemea msaada wa serikali na kuwafanya wawe wajasiria mali.