Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado hakuna usawa baina ya weusi na wazungu Afrika Kusini:Kamati

Bado hakuna usawa baina ya weusi na wazungu Afrika Kusini:Kamati

Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utesaji imekamilisha kujadili ripoti ya Afrika ya Kusini kuhusu utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa utokomezaji wa mifumo yote ya ubaguzi wa rangi. Flora Nducha na maelezo kamili.

(TAARIFA YA FLORA)

Akiwasilisha ripoti hiyo Naibu Waziri wa Sheria na Maendeleo ya  Katiba wa Afrika ya Kusini, John Jeffery amesema kukata mizizi ya ubaguzi wa rangi nchini humo ni zaidi ya kufuta sheria za ubaguzi wa rangi na kuzibadilisha na zile za kuleta usawa na utawala wa sheria.

Amesema kufanikisha hilo kunahitaji utashi wa kisiasa , rasilimali, ujenzi wa taasisi mpya za kuunga mkono demokrasia na kuendelea kutambua mtazamo wa kitaifa wa haki za kijamii na kiuchumi kwa wote. Hata hivyo amesema hatua zimepigwa katika kujaribu kuinua hali ya maisha ya kila raia .

(SAUTI YA JOHN JEFFEERY)

"Kwa hivyo tunatoa tamko madhubuti ya kuwa Afrika Kusini ni taifa la watu wa aina mbili, watu weupe wenye mafanikio makubwa katika maisha bila kujali jinsia yao na jeographia, na lingine lililokua kubwa zaidi ni la watu weusi walio masikini na waathirika wakubwa ni wanawake wa mashinani."

Nayo kamati imeitaka serikali ya nchi hiyo kuhakikisha hatua inazochukua zinakwenda sanjari na mikataba ya haki ya kimataifa na mapendekezo ya kamati dhidi ya utesaji, ikiongeza kuwa, bado kuna ubaguzi wa wazi baina ya weusi walio wengi na wazungu wachache nchini humo. Pia ikitaja hofu yake kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya wageni, na hali ya kutovumiliana.