Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yaridhia ratiba ya mchakato wa uchaguzi 2016

Somalia yaridhia ratiba ya mchakato wa uchaguzi 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha tangazo lililotolewa nchini Somalia leo na jopo la utekelezaji wa uchaguzi nchini humo, (FIEIT) kuhusu ratiba ya uchaguzi wa kitaifa.

Uamuzi huo umetangaza kuwa uchaguzi wa wabunge wa kitaifa utafanyika kati ya tarehe 24 Septemba na Oktoba 10, ihali ule wa Rais ukitarajiwa uwe umefanyika ifikapo tarehe 30 mwezi huo wa Oktoba.

Taarifa ya msemaji wa Ban imesema uamuzi huo tayari umeridhiwa na jukwaa la uongozi wa kitaifa nchini Somalia.

Katibu Mkuu amesema ni matumaini yake kuwa ratiba hiyo iliyokubaliwa itazingatiwa na ametaka pande zote kujizuia na vitendo vyovyote vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wake.

Amesema mchakato wa uchaguzi mwaka huu wa 2016 nchini Somalia ni muhimu katika kukamilisha safari ya kusaka demokrasia.

Hivyo amepongeza hatua ya jukwaa hilo la uongozi ya kuazimia kuwepo kwa kipindi cha mpito cha mfumo wa vyama vingi vya siasa ifikapo mwaka 2018 kabla ya uchaguzi mwaka 2020.

Amesisitiza umuhimu wa uchaguzi huo kufanyika kwa uhuru, haki na uwazi na kuzingatia haki za binadamu.