Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNRWA azuru Syria kwa mara ya pili mwaka huu

Mkuu wa UNRWA azuru Syria kwa mara ya pili mwaka huu

Kamishina Mkuu wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina(UNRWA) , Pierre Krähenbühl amezuru Syria tarehe 6-8 Agosti, na kukutana na wakimbizi wa Kipalestina, wafanyakazi wa UNRWA na maafisa wa serikali.

Katika ziara yake hiyo ya pili kwa mwaka huu, kamishina mkuu ameshuhudia hali ya usalama na hofu ya ulinzi kwa wakimbizi wa Kipalestina na wafanyakazi wa UNRWA hasa katika wakati huu ambapo vita nchini Syria vinaendelea kuwaweka raia katika hatari kubwa kwenye maeneo ya Aleppo , Khan Eshieh, Yarmouk-Yalda, na sehemu za jimbo la Dera’a .

Bwana Krähenbühl amesema ni muhimu kwamba madhila yote na jinamizi lililoletwa na kushuhudia vifo vingi vya raia na majeruhi limalizwe kama sehemu ya suluhu ya kisiasa ya mzozo huo.

Bwana Krähenbühl pia amepongeza kazi nzuri inayofanywa na wafanyakazi wa UNRWA Damascus, Aleppo, Hama, Homs, Latkia na Dera'a na kuendelea kujitolea kwa wafanyakazi hao kusaidia wakimbizi wa Kipalestina licha ya hatari na mazingira ya vita vinavyoendelea.