Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Aleppo yameathiri zaidi huduma za afya- WHO

Machafuko Aleppo yameathiri zaidi huduma za afya- WHO

Wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana leo kuhusu hali huko Aleppo, Syria, imeelezwa kuwa kuzingirwa kwa mji huo kumevuruga utoaji wa huduma za afya, huku mahitaji ya huduma hizo yakiongezeka, hususani kutokana na majeraha yanayosababishwa na vita, limesema Shirika la Afya Duniani (WHO). Amina Hassan na taarifa kamili.

Taarifa ya Amina

WHO imesema vituo vingi vya afya havifanyi kazi kutokana na mashambulizi, upungufu wa wahudumu wa afya, na upungufu wa dawa na vifaa tiba vingine vinavyohitajika. Tarik Jasarevic ni msemaji wa WHO

(SAUTI YA TARIK)

“Takribani wahudumu sita wa afya wameuawa mjini Aleppo kutokana na mashambulizi kwenye vituo hivyo 2016, na kupunguza zaidi idadi ya wataalamu wa afya, ambayo tayari ni ndogo. Kwa kila daktari mmoja anayeuawa au kukimbia, zaidi ya Wasyria 40 wananyimwa huduma ya afya kwa siku”