Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanalipa gharama kubwa katika mzozo wa Yemen: UNICEF

Watoto wanalipa gharama kubwa katika mzozo wa Yemen: UNICEF

Watoto wanne wamearifiwa kuuawa na wengine watatu kujeruhiwa Agosti 7 kwenye wilaya ya Nihm, mashariki mwa mji mkuu wa Yemen, Sana’a.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limelaani vikali vitendo hivyo na kuzitaka pande zote katika mzozo wa Yemen kuwa waangalifu na kuepuka miundombinu inayotoa huduma kwa raia kama vile shule na hospitali. Watoto nchini Yemen wanalipa gharama kubwa ya maisha yao katika mzozo huu amesema Julien Harneis mwakilishi wa UNICEF nchini humo.

Ameongeza kuwa tangu kufurumuka kwa machafuko nchini Yemen Machi 2015 UNICEF imeweza kuthibitisha kwamba watoto 1,121 wameuawa na wengine 1650 kujeruhiwa, huku akionya kwamba idadi kamili huenda ikawa kubwa zaidi.

UNICEF imezitaka pande zote kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuhakikisha zinawalinda watoto.