Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa Argentina, Ban akutana na Rais Macri, wajadili mambo mseto

Akiwa Argentina, Ban akutana na Rais Macri, wajadili mambo mseto

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani nchini Argentina, amekutana leo na kufanya mazungumzo na Rais wa Argentina, Mauricio Macri, ambapo wamejadili kuhusu masuala mseto yanayohusu Umoja wa Mataifa na taifa la Argentina, na jinsi ya kuimarisha ubia kati ya taifa hilo na Umoja wa Mataifa.

Katika mkutano baadaye na wanahabari, Ban amesema kuwa baadhi ya masuala waliyomulika ni ulinzi wa amani, mabadiliko ya tabianchi, usawa wa jinsia, na masuala ya kikanda. Kuhusu suala la jinsia, Ban amepongeza uongozi wa Rais Macri katika hatua ya hivi karibuni ya kuzindua mpango wa kitaifa wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Kuhusu tabianchi, Ban amesema amemshukuru Rais Macri kwa dhamira ya Argentina katika kutekeleza mkataba wa Paris kuhusu tabianchi, na tangazo la rais huyo kwamba Argentina inaenda kuuridhia mkataba huo haraka iwezekanavyo.

Kuhusu ulinzi wa amani, Katibu Mkuu amepongeza ushiriki wa Argentina katika ulinzi wa amani, hususan katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia.

Aidha, ameipongeza Argentina kwa mshikamano na dhamira yake katika kuendeleza haki za binadamu, na katika masuala ya kibinadamu.