Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi Sudan Kusini wamenihadaa- Bangura

Viongozi Sudan Kusini wamenihadaa- Bangura

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono vitani, Zainab Hawa Bangura amesema amechukizwa na kile kilichotokea Sudan Kusini kufuatia mapigano ya mwezi Julai yaliyosababisha vifo na ubakaji wa wanawake na wasichana.Taarifa zaidi na Brian Lehander.

(Taarifa ya Brian)

Akihojiwa na Radio Miraya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, Bi. Bangura amesema mara kwa mara amekuwa na mazungumzo na Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar kuhusu ulinzi wa raia lakini bado mapigano hayo yalitokea mwezi Julai na kuleta madhila hayo.

(Sauti ya Bangura)

“Siyo tu kwamba nimesikitishwa, bali pia nimekasirishwa sana kwa sababu unafahamu mimi ni mwanamke wa kiafrika na nimeona vile ambavyo wanawake hawa wamekumbwa na machungu Sudan Kusini.”

Bi. Bangura amesema atapigania haki za wanawake hao hadi tone la mwisho la uhai wake akisema..

(Sauti ya Bangura)

“Hao watu ambao wanadhani watakwepa adhabu watakuwa wanachekesha, kwa sababu tutawafuatilia! Haijalishi ni akina nani na wako wapi! Tutawasaka na tutawawajibisha kwa uhalifu huu, hawatatokomea hivi hivi.”