Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani wa UM auawa Mali, wanne wajeruhiwa

Mlinda amani wa UM auawa Mali, wanne wajeruhiwa

Mlinda amani mmoja wa Umoja wa Mataifa ameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa baada ya bomu la kutengenezwa kulipua msafara wao kwenye eneo la Aguelhok, mjini Kidal.

Kufuatia taarifa za shambulio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani kitendo hicho ambacho kinafuatia shambulio la aina hiyo tarehe Tano mwezi huu kwenye viunga vya Kidal.

Ban kupitia msemaji wake ameeleza kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa na ametoa wito kwa wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Hata hivyo amesema mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani hayatokatisha tamaa harakati za kusaidia serikali ya Mali na wadau wake kutekeleza makubaliano ya amani.

Katibu Mkuu ametua salamu za rambirambi kwa wafiwa na serikali ya Mali na kutakia ahueni ya haraka majeruhi huku akikumbusha wananchi wa Mali kuwa wajbu wa kuleta amani unasalia mikononi mwao hivyo wajizatiti kuleta amani ya nchi yao.