Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Yemen zakutana Kuwait na kuna nuru ya makubaliano- Ould

Pande kinzani Yemen zakutana Kuwait na kuna nuru ya makubaliano- Ould

Mazungumzo kuhusu Yemen yamehitimishwa huko Kuwait ikielezwa kuwa yamekuwa na mafanikio hasa kwa kitendo cha pande mbili kinzani kwenye mzozo huo kuweza kukaa kwenye meza moja na kujadili masuala ya siasa, ulinzi na ubinadamu nchini mwao.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed akizungumza na wahabari mjini Kuwait baada ya mazungumzo hayo amesema masuala magumu yalijadiliwa na wajumbe kutoka upande wa serikali na wale wa kikundi cha People’s Congress na Ansar.

Amesema mazungumzo hayo yameweka nuru ya uwezekano wa kupatikana kwa makubaliano hivi karibuni huku akitaka watu wanaochochea au wanaoingilia masuala ya ndani ya Yemen kuacha mara moja kwani wanazidi kuzorotesha matumaini ya amani.

Bwana Ahmed amesema pande mbili hizo zimeibuka na taarifa yenye vipengele kumi ikiwemo kuendelea na mashauriano, kujiepusha na vitendo vinavyoweza kukwamisha kufikiwa kwa makubaliano na kufanikisha kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa namba 2216 la mwaka jana.