Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kimataifa yaahidi kufikisha msaada wa kuokoa maisha Kaskazini mwa Nigeria- OCHA

Jumuiya ya kimataifa yaahidi kufikisha msaada wa kuokoa maisha Kaskazini mwa Nigeria- OCHA

Kaimu Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa OCHA nchini Nigeria Munir Safieldin , amekamilisha ziara ya wiki moja kutathimini hali ya kibinadamu Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo kufuatia shambulio dhidi ya msafara wa misaada ya kibinadamu kwenye jimbo la Borno Julai 28.

Bwana Safieldin katika ziara yake amekutana na mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs na mashirika yote ya Umoja wa mataifa yanayotoa msaada katika eneo hilo, na pia kuzungumza na viongozi wa serikali jimbo la Borno na mratibu wa masuala ya kibinadamu wa jimbo hilo bwana Alhaji Usman Shuwa Jidda.

Pia mratibu huyo amezuru kambi mbalimbali za wakimbizi wa ndani hasa eneo la Maiduguri na kushuhudia kazi za mashirika ya kibinada za kufikisha msaada unaohitajika kuokoa maisha ya maelfu ya watu.

Licha ya shambulio la karibuni dhidi ya msafara wa kutoa misaada mashirika yasiyo ya kiserikali na Umoja wa mataifa wameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine kufikisha msaada huo muhimu wa kibinadamu.