Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Michezo ya Olimpiki yaanza leo Rio, wakimbizi wawakilishwa

Michezo ya Olimpiki yaanza leo Rio, wakimbizi wawakilishwa

Michezo ya Olimpiki ya Rio2016 inaanza rasmi leo Agosti Tano jijini Rio Brazil, ikishirikisha timu ya wakimbizi kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya michezo hiyo.

Timu hiyo ya wakimbizi inajumuisha wapiga mbizi wawili kutoka Syria, wacheza mieleka wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mkimbiaji wa marathon kutoka Ethiopia, na wakimbiaji watano wa masafa ya wastani kutoka Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi (UNHCR), tukio hilo la kihistoria linatokea wakati watu milioni 65.3, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi ya watu katika historia, wanalazimika kukimbia makwao kwa sababu ya migogoro na utesaji.

William Spindler ni msemaji wa UNHCR, Geneva..

“Timu ya wakimbizi ya Olimpiki inatumai kuupa ulimwengu taswira ya uthabiti wa wakimbizi na vipaji vyao ambavyo havijatambuliwa. Kamishna Mkuu wa UNHCR atakuwa Rio kushangilia timu hiyo.”