Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

China yafanya majaribio ya basi la kipekee

China yafanya majaribio ya basi la kipekee

Mradi wa usafiri wa umma nchini China wenye lengo la kupunguza msongamano wa magari mijini sambamba na uchafuzi wa hali ya hewa umefanyiwa majaribio wiki hii kwenye jimbo la Hebei.

Mradi huo wa mabasi ya abiria yaliyonyanyuliwa juu, TEB na ambayo yanatumia nishati ya umeme, unahusisha mabasi ambayo katikati ya njia ya kuwezesha magari madogo kupita wakati safari zake zikiendelea.

Urefu wa ulalo wa basi hilo la nyakati zijazo ni mita 22, upana wake ni mita 7.8 ilhali urefu kwenda juu ni mita 4.8.

Tovuti ya mabadiliko ya tabianchi inayochapisha taarifa kuhusu miradi ya kupunguza uchafuzi wa mazingira huku ikiungwa mkono na shirika la mazingira duniani, UNEP imesema basi hilo lina uwezo wa kubeba abiria 300 sawa na mabasi 40 ya kawaida.

Mhandisi mkuu wa mradi huu Song Youzhou, anaamini kuwa basi la aina hiyo lina uwezo wa kupunguza tani 2,500 za hewa ya ukaa sambamba na msongamano mkubwa wa magari nchini China.

Basi hilo linatarajiwa kufikia kasi ya kilometa 60 kwa saa likipita kwenye njia maalum za reli zilizotandazwa katika barabara za kawaida.

Hata hivyo hadi sasa haijafahamika ni kwa jinsi gani mfumo huo utaweza kufanya kazi na malori au magari yenye urefu zaidi kuliko basi hilo.