SPLA imetekeleza ukiukaji mkubwa wa haki Sudan Kusini: Zeid

SPLA imetekeleza ukiukaji mkubwa wa haki Sudan Kusini: Zeid

Uchunguzi wa awali wa Umoja wa mataifa kuhusu mapigano ya karibuni Sudan Kusini  na matokeo yake umeonyesha kwamba vikosi vya ulinzi na usalama vya serikali  vimetekeleza mauaji, ubakaji , uporaji na uharibifu. Hiyo kauli ya mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa aliyotoa leo alhamisi, huku akitoa wito kwa baraza la usalama kuchukua hatua kali. Flora Nducha na taarifa kamili.

(TAARIFA YA FLORA)

Zeid Ra’ad Al Hussein, amesema mvutano bado ni mkubwa na ukiukaji unaendelea Juba na katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Mkuu huyo wa haki za binadamu amewasilisha ripoti kwa baraza la usalama ya matokeo ya awali ya uchunguzi wa siku tano za mapigano yaliyoanza mji mkuu Juba Julai 7 na matokeo ya machafuko hayo.

Ameongeza kuwa taarifa zilizopokelewa na ofisi yake zinaonyesha mamia ya wapiganaji na raia waliuawa kwenye mapigano hayo huku baadhi ya raia wakiuawa na jeshi la serikali SPLA hasa wale wenye asili ya Nuer. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

"Nafikiri ni kwa  kukabiliana na ukwepaji sheria kwani kunakua na mzunguko wa ukatili  Sudan Kusini  mara kwa mara, na kama nilivyosema watu hawawajibishwi,  pasipokuwepo adhabu kali na wapiganaji kukamatwa na kuwekwa ndani kwa makosa makubwa ya jinai, kwa kuzingatia ushahidi sahihi , basi tabia hii itaendelea"