Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

O’Brien alaani ghasia dhidi ya raia na wahudumu wa misaada Sudan Kusini:

O’Brien alaani ghasia dhidi ya raia na wahudumu wa misaada Sudan Kusini:

Msaidizi wa Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa katika masuala ya kibinadamu na kuratibu misaada ya dharura Stephen O’Brien, amekamilisha ziara ya siku tatu nchini Sudan Kusini hii leo, kwa wito kwa pande zote katika mzozo kutekeleza wajibu wao wa kuwalinda raia, hasa katika machafuko mapya yaliyotawanya maelfu ya watu katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

O’Brien amesema watu wa Sudan Kusini wameteseka vya kutosha na kwa muda mrefu, na kuongeza kuwa amesikitishwa na vitendo vya kikatili vinavyotekelezwa dhidi ya raia vikiwemo vinavyofanywa na wanajeshi na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomesha madhila hayo na kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sheria.

O’Brien ambaye amezuru maeneo mbalimbali na kukutana na waathirika wa vita, ikiwemo Wau, Juba na Aweil amesema hali nchini humo ni mbaya sana na ulinzi kwa raia ndio suala la kupewa kipaumbele, hasa kukiwa na ripoti za ubakaji na ukatili mwingine wa kingono baada ya kuzuka upya machafuko ikiwemo Juba na Wau.

Hadi sasa watu milioni 2.8 wameshafikiwa na msaada wa kibinadamu na ulinzi, hata hivyo mpango wa usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2016 umefadhili asilimia 40 pekee na kuacha pengo la dola milioni 765.