Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WaSudan Kusini waliofungasha virago kukimbia nchi jirani sasa ni 60,000:UNHCR

WaSudan Kusini waliofungasha virago kukimbia nchi jirani sasa ni 60,000:UNHCR

Jumla ya watu 60,000 wamekimbia Sudan Kusini tangu kuzuka kwa machafuko ya karibuni na kwenda nchi jirani za Kenya na Uganda. Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR wanaoingia Uganda idadi yao imeongezeka mara mbili huku tangu Desemba mwaka 2013 sasa jumla ya watu waliokimbilia nchi jirani ni 900,000.

Uganda imeshapokea wakimbizi 52,000 katika kipindi cha wiki tatu, wakati Kenya imepokea 1000 na Sudan 7000 kwa kipindi hichohicho. Hata hivyo taarifa zinasema makundi ya watu wenye silaha yaliyo kwenye barabara iendayo Uganda yanajaribu kuzuia watu kukimbia kutoka Sudan Kusini.

UNHCR inasema juhudi zinafanyika hivi sasa kufungua kambi mpya ya wakimbizi yenye uwezo wa kuhifadhi watu 100,000 kwenye wilaya ya Yumbe nchini Uganda.

Kenya na Uganda zote zimeripoti visa vya utapia mlo hasa miongoni mwa watoto wanaowasili, na walio wagonjwa wanawekwa katika mpango maalumu wa lishe ili kuokoa maisha yao.