Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahofia mahitaji ya kiafya huku kipindupindu kikisambaa Sudan Kusini

WHO yahofia mahitaji ya kiafya huku kipindupindu kikisambaa Sudan Kusini

Shirika la afya duniani (WHO) limeelezea hofu yake dhidi ya mahitaji ya jumla ya kiafya Sudan Kusini hususani kwa wakimbizi wa ndani. Joshua Mmali na maelezo zaidi.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Shirika hilo limesema mlipuko wa kipindupindu umeshakatili maisha ya watu 21 hadi sasa kuna visa 586 vilivyoripotiwa nchini humo. Hospitali kuu ya Juba inapokea na kulaza wagonjwa wapya wa kipindupindu 35 kila siku.

Limeongeza kuwa mlipuko wa kipindupindu umeongeza adha ya kiafya kwa nchi hiyo ambayo tayari ina madhila mengine huku fedha zikihitajika haraka kukidhi mahitaji, kama anavyofafanua msemaji wa WHO Fadela Chaib

(SAUTI YA FADELA CHAIB)

“Sudan Kusini ina vyanzo vikuu vitatu vya vifo hasa kwa watoto, kwanza Malaria, matatizo ya kupumua la pili na kipindupindu la tatu. Kwa bahati mbaya pia kuna visa vingi vya watoto wenye utapia mlo na hali ni ya hatari sana”

Ameongeza kuwa fedha za ufadhjili dola milioni 17.5 zinahitajika haraka kukidhi mahitaji hayo ya kiafya.