Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na OSCE walaani ukandamizaji wa wanahabari Uturuki

UM na OSCE walaani ukandamizaji wa wanahabari Uturuki

Wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya (OSCE), wamelaani vitendo vya serikali ya Uturuki vya kukandamiza wanahabari na vyombo vya habari nchini humo, kufuatia jaribio la kuipindua serikali.

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kujieleza, David Kaye, na Mwakilishi wa OSCE kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Dunja Mijatoviæ, wameeleza kusikitishwa na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na mamlaka za Uturuki, zikiwemo kuwakamata makumi ya wanahabari na kufunga idadi kubwa ya vyombo vya habari katika saa 24 zilizopita.

Wawili hao wameonya kuwa vitendo hivyo ni pigo kubwa dhidi ya uhuru wa umma kujieleza na kuwajibishwa kwa serikali. Kwa mantiki hiyo, wameisihi serikali ya Uturuki kutathmini tena uamuzi huo na kutimiza wajibu wao wa kulinda uhuru wa vyombo vya habari.

Ripoti zinasema kuwa serikali ya Uturuki iliamuru kufungwa vituo 16 vya televisheni, 23 vya redio, magazeti 45, na majarida 15.