Jamuhuri ya Korea na UNESCO kuimarisha sekta ya utamaduni na filamu Uganda

Jamuhuri ya Korea na UNESCO kuimarisha sekta ya utamaduni na filamu Uganda

Wakati Afrika Mashariki inaibuka kwa kasi kama moja ya maeneo yenye ubunifu na ujasiriamali duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu na utamaduni, UNESCO linazindua leo Julai 27 2016 nchini Uganda, mradi mpya ili kuimarisha sekta ya utamaduni na ujuzi wa wataalamu wa ubunifu, kwa msaada wa fedha wa Jamhuri ya Korea.

Mradi huu, wa ubunifu wa sekta ya utamaduni na maendeleo , unaimarisha ubunifu endelevu nchini Uganda na kusaidia katika utekelezaji wa mkataba wa 2005 wa kulinda na kuchagiza tamaduni tofauti.

Uganda tayari imeshatambulika kama kituo cha sekta ya filamu , ilipotumika wakati wa kurekodi filamu ya Hollywood iitwayo Mississippi Masala, ikichezwa na nyota wa filamu Denzel Washington na kuongozwa na mtayarishaji Mira Nair.

Bi Nair pia ameanzisha shule ya filamu Kampaka iitwayo Maisha Film Lab ikitoa mafunzo kwa waongozaji chipukizi , waandishi wa filamu na watayarishaji kutoka Uganda, Kenya, Rwanda na Tanzania.