Unyanyasaji wa kingono unaathiri kila sehemu ya maisha- Jane Holl Lute
Mratibu maalum kuhusu kuboresha jitihada za Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na unyanyasaji wa kingono, Jane Holl Lute, amesema unyanyasaji wa kingono ni tatizo linaloathiri kila sehemu ya maisha, na hivyo inapaswa kutambuliwa kwamba ni tatizo la kimataifa linaloathiri hata Umoja wa Mataifa. Taarifa kamili na Joseph Msami.
Taarifa ya Msami
Katika Mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, Bi Lute amesema kufanya utambuzi huo ndio mwanzo wa kumakinika na kuboresha mfumo wa Umoja wa Mataifa ili uweze kuzuia unyanyasaji wa kingono usitokee, na kukabiliana nao haraka pale unapojitokeza.
Hata hivyo, amesema inasikitisha hasa zaidi pale walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanapodaiwa kufanya vitendo vya unyanyasaji wa kingono
“Inasikitisha zaidi unapotendwa na walinda amani kwa sababu ya imani waliyo nayo watu kwa walinda amani na kwa Umoja wa Mataifa, wahudumu wa maendeleo, na wahudumu wa kibinadamu, kwani wametumwa kule kuwalinda hawa watu. Nadhani kila unapokuwa na madai ya tabia mbovu kama hii, ina athari nyingi. Bilas haka inatia doa sifa ya Umoja wa Mataifa."