Skip to main content

IOM yakubaliwa kuwa shirika linalohusiana na Umoja wa Mataifa

IOM yakubaliwa kuwa shirika linalohusiana na Umoja wa Mataifa

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kupitia Baraza Kuu la Umoja huo, leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la kuridhia makubaliano yanayolifanya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kuwa shirika linalohusiana na umoja huo.

Makubaliano hayo yanaainisha uhusiano wa karibu kati ya IOM na Umoja wa Mataifa katika kuimarisha ushirikiano na uwezo wao kutimiza majukumu yanayowanufaisha wahamiaji na nchi wanachama.

Kupitia makubaliano hayo, Umoja wa Mataifa unaitambua IOM kama mdau adhimu katika nyanja ya uhamiaji wa watu.

Umuhimu wa ushirikiano na IOM unatambuliwa katika masuala kadhaa, yakiwemo kuwalinda wahamiaji na watu waliolazimika kuhama makwao katika jamii zilizoathiriwa, kuwatafutia makazi wakimbizi na kuwarejesha kwa hiari, pamoja na kujumuisha uhamiaji katika mipango ya nchi ya maendeleo.

Makubaliano hayo yatatiwa saini na Katibu Mkuu, Ban Ki-moon, na Mkurugenzi wa IOM, William Lacy Swing, wakati wa mkutano kuhusu wakimbizi na wahamiaji, mnamo Septemba 19, 2016.