Skip to main content

Tunahitaji kuimarisha tena kasi ya ulinzi na kuwafikia raia Syria- O’Brien

Tunahitaji kuimarisha tena kasi ya ulinzi na kuwafikia raia Syria- O’Brien

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Stephen O’Brien, ametoa wito iimarishwe tena kasi iliyoanzishwa mwanzoni mwa mwaka 2016 kuhusu ulinzi na ufikishaji misaada kwa raia wenye uhitaji nchini Syria, na kutaka pia vitendo vya kuwazingira raia vikomeshwe mara moja.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limekutana kujadili hali Mashariki ya Kati, O’Brien amesema kasi iliyowekwa katika miezi sita ya kwanza yam waka huu na baada ya kuundwa kwa kikosi-kazi cha kimataifa kuhusu usaidizi kwa Syria, inapaswa iwe msingi wa kubadili hali ya ulinzi na ufikishaji misaada kwa raia hadi mwishoni mwa mwaka.

“Kote nchini Syria, watu wapatao milioni 5.5 wenye uhitaji walioko katika maeneo magumu kufikia na yaliyozingirwa, wanapata usaidizi mdogo sana wa ulinzi na ule wa kuokoa maisha.”

O’Brien amesema kati yao, watu 590,000 wamenaswa kabisa katika maeneo yaliyozingirwa, na kusimulia Baraza hilo hali ilivyo kwa wanaoishi katika maeneo hayo.

“Kwa wingi watu hawa wanasaka njia za kukwepa mapigano ya kila siku, ulipuaji mabomu, na risasi za walenga shabaha zinazoyaghubika maisha yao. Wazazi hawana chakula cha kuwapa watoto wao wenye njaa. Utapiamlo umekithiri hadi watoto wanafariki. Hakuna maji safi wala umeme. Bei za bidhaa chache zinazofikia maeneo hayo zimepanda kwa kiwango kikubwa, na watu hawawezi kuzimudu. Ni mahali penye uhaba wa elimu, na penye ukatili wa kingono, utumikishaji wa watoto na ndoa za utotoni.”

Akitaja hatua zinazopaswa kuchukuliwa, O’Brien ametoa wito uhasama wote usitishwe tena, na mashambulizi holela yanayoua raia yakomeshwe. Aidha, ametaka hatua zote mwafaka zichukuliwe na pande kinzani kuhakikisha kuwa raia wanafikiwa na usaidizi wa kibinadamu kwa njia salama, endelevu, na bila masharti.