Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu kuzingatia utawala wa sheria hasa sasa Uturuki:Ban

Ni muhimu kuzingatia utawala wa sheria hasa sasa Uturuki:Ban

Kufuatia tangazo la hali ya dharura kwa miezi mitatu nchini Uturuki, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, amesema anatambua hakikisho lililotolewa na viongozi waandamizi wa serikali ya Uturuki kuhusu uzingatiaji kamili wa utawala wa sheria na mchakato wa wakati wa kuchunguza na kuwafungulia mashitaka wale wanaoonekana kuwajibika na jaribio la mapinduzi la tarehe 15-16 Julai.

Ban amesema hii ni muhimu hasa baada ya tangazo la hali ya dharura na kuendelea kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kusimamishwa kazi kwa watu. Ban ameutaka uongozi wa Uturuki kuzingatia hakikisho ililotoa na kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha katiba inafuatwa, na sheria za kimataifa za haki za binadamu zinaheshimiwa sanjari na wajibu wa kimataifa wa serikali hiyo.

Hayo yanajumuisha uhuru wa kujieleza, kutembea na kukusanyika kwa amani, lakini vilevile uhurua wa mfumo wa sheria, wafanyakazi wa mahakama na mchakato mzima kuzingatia haki.

Ameongeza kuwa anatumai mchakato mzima wa hali ya dharura utafanyika kwa kuzingatia uwazi.