Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulizi dhidi ya watoto Syria- UNICEF

Hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulizi dhidi ya watoto Syria- UNICEF

Mwakilishi wa Shirika la Kuhdumia Watoto (UNICEF) nchini Syria, Hanaa Singer, amelaani vitendo vyote vya kikatili dhidi ya raia nchini Syria, na kutaka pande kinzani katika mzozo wa Syria kutimiza wajibu wao wa pamoja wa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, ambazo zinalinda watoto.

Aidha, ameongeza kuwa hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha mashambulizi dhidi ya watoto, kufuatia kuuawa kwa watoto 20 katika shambulio la angani, na kuuawa mvulana mwenye umri wa miaka 12 mjini Aleppo, mbele ya kamera.

Kwa mujibu wa wadau wa Umoja wa Mataifa walioko mashinani, familia kutoka kijiji cha Tukhar karibu na Manbij, yapata kilomita 80 kutoka Aleppo, zilikuwa zinajiandaa kukimbia kijiji hicho wakati ziliposhambuliwa kutoka angani.

Juliette S. Touma ni afisa mkuu wa mawasiliano katika Ofisi ya UNICEF Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika

“Watoto wanaendelea kuuawa Syria karibu kila siku kutokana na vita nchini Syria. Na tunachotambua ni kwamba vita nchini Syria vimekuwa katili hata zaidi, na kuwaacha watoto katikati ya vita hivyo, na watoto wanaathiriwa zaidi katika vita hivyo ambavyo hawakuchangia kabisa.”

UNICEF inakadiria kuwa watoto wapatao 35,000 wamenaswa Manbij na maeneo ya karibu, na hawana mahali salama pa kukimbilia. Katika wiki sita zilizopita, zaidi ya watu 2,300 wameripotiwa kuuawa katika eneo hilo, wakiwemo watoto wengi.