Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 284 zahitajika kwa ajili ya msaada wa kibinadamu Mosul:OCHA

Dola milioni 284 zahitajika kwa ajili ya msaada wa kibinadamu Mosul:OCHA

Ombi la dola milioni 284 kwa ajili ya kufadhili msaada wa kibinadamu limezinduliwa leo kabla ya kampeni inayotarajiwa ya serikali ya Iraq ya kuurejesha mji wa Mosul katika udhibiti wake. Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa mataifa nchini Iraq, Lise Grande,amesema watu takribani milioni 1.5 wanaweza kuathirika na kuna uwezekano athari zikawa kubwa mno.

Umoja wa mataifa na washirika wa masuala ya kibinadamu wameonya kwamba muda unawatupa mkono wa kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya operesheni za kijeshi za kufurusha kukdi la kigaidi laISIL, au Daesh, ambalo limekuwa likishikilia mji wa Mosul tangu Julai mwaka 2014.

Bi Grande ameongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa vifo vingi vya raia na familia zitakazojaribu kukimbia zitakuwa katika hatari kubwa. Amesema endapo ufadhili wa fedha za ziada hazitopatikana haraka , basi itakuwa vigumu kwa operesheni za kibinadamu kutoa msaada muhimu unaohitajika.