Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni lazima tuzuie, tujiandae, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi- Ban

Ni lazima tuzuie, tujiandae, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa changamoto za jitihada za kukabiliana na athari za El Nino ni zaidi ya mzigo wa kibinadamu, kwani majanga ya hali ya hewa huvuruga ufanisi wa maendeleo.

Ban amesema hayo wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu El Nino na tabianchi, ambao umefanyika leo Jumanne kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu ameongeza kwamba watu na jamii haziwezi kujikomboa kutoka kwa umasikini au njaa, iwapo rasilmali zao zinaharibiwa na mafuriko, vimbunga au ukame kila baada ya miaka michache.

“Hata utapiamlo unapotibiwa na maisha ya watoto kuokolewa, wanaweza kuathiriwa katika maisha yao yote kwa sababu ya kudumaa na kulemazwa wanapokua. Hili huathiri vibaya elimu, uwezo wa watu kujipatia riziki, na fursa za jamii na mataifa kupata ufanishi na maendeleo kwa njia endelevu.”

Ban amesema, kwa wengi wa watu maskini zaidi, majanga ya hali ya hewa yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi huenda yakahatarisha utimizaji wa Ajenda yam waka 2030 ya maendeleo endelevu.

“Changamoto hii mpya inahitaji mabadiliko mapya katika jinsi tunavyofanya kazi. Ni muhimu tujifunze kutokana nah ii El Nino. Ni lazima tuzuie, tujiandae, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambayo yana madhara makubwa zaidi kwa wale walioyasababisha kwa kiwango kidogo zaidi.”