Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yalaani mashambulizi katika hospitali Syria

WHO yalaani mashambulizi katika hospitali Syria

Shirika la afya duniani WHO limelaani vikali mashambulizi kwenye hospitali majimbo ya Aleppo na Idleb nchini Syria, na limetuma salamu za rambirambi kwa familia, wafanyakazi wenzao wa huduma za afya na wagonjwa waliouawa kwenye mashambulizi hayo.

Mwishoni mwa juma hospitali ya Omar Ibn Abdel Aziz, mashariki mwa Aleppo ilishambuliwa na wahudumu wengi wa afya wakajeruhiwa na uharibifu mkubwa kufanyika. Hospitali hiyo imeshambuliwa mara tatu katika kipindi cha siku 45 kati ya Juni na Julai.

Pia tarehe 11 Julai hospitali nyingine inayosimamiwa na serikali Idleb ilishambuliwa na watu watatu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Kwa mujibu wa WHO mashambulizi haya ya karibuni ni pigo kubwa kwa jamii ambazo tayari zimeshaathirika na vita nchini Syria.

Kwa mujibu wa WHO kumethibitishwa mashambulio 40 dhidi ya vituo vya afya nchini Syria kwa mwaka huu pekee, huku asimilia 60 ya hospitali na vituo vya afya vya umma ama vimefungwa au hutoa huduma nusu.