Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uhusiano kati ya kutenda wema na kutenda vyema- Eliasson

Kuna uhusiano kati ya kutenda wema na kutenda vyema- Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema leo kuwa sekta binafsi ina uwezo wa kuathiri moja kwa moja maisha ya watu, na wajibu mkubwa katika kuwezesha maisha bora.

Bwana Eliasson amesema hayo wakati akihutubia jukwaa la wafanyabiashara kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

Naibu Katibu Mkuu amesema, kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kutenda wema na kutenda vyema, akiongeza kuwa biashara bora ni zile zinazowekeza katika mustakhbali unaojali mazingira, kupanua masoko, kuongeza faida na kuboresha jamii.

“Kuna njia nyingi ambazo kazi yenu inaweza kufaidi SDGs. Mnaweza kuleta nishati mbadala kwa jamii. Mnaweza kuboresha mazao ya kilimo kwa wakulima wadogowadogo. Mnaweza kupanua masoko au bidhaa na huduma, na kufikia watu walio mbalo vijijini na hatarini. Mnaweza kubadili mitandao ya thamani ili iwe endelevu zaidi. Mnaweza kuwezesha na kukuza biashara. Kwa njia hizi, mnaweza kusaidia kujenga jamii zilizo jumuishi na thabiti zaidi.”

Eliasson amesema njia zote hizo zinachangua moja kwa moja amani na usalama, pamoja na maisha bora na ukuaji wa uchumi.

“Malengo ya SDGs yameoanishwa na yanawezeshana. Kwa njia moja, yanawakilisha tangazo la uhuru katika ulimwengu wetu wa pamoja. Ili kuyafikia malengo hayo, tunahitaji ubunifu na uvumbuzi katika sekta binafsi.”