Skip to main content

Maelfu ya watu wakimbilia Uganda kufuatia machafuko Sudan Kusini

Maelfu ya watu wakimbilia Uganda kufuatia machafuko Sudan Kusini

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), limesema idadi ya watu wanaotafuta makazi na usalama nchini Uganda kutoka Sudan Kusini imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika siku chache zilizopita, kufuatia hali tete katika taifa hilo changa zaidi duniani.

Zaidi ya watu 1,300 walivuka mpaka na kuingia Uganda kati ya Ijumaa na Jumamosi wiki iliyopita, na wengine zaidi ya 1,600 wakawasili Jumapili.

Kabla ya Ijumaa, idadi ya wastani ya waliowasili Uganda kila siku kutoka Sudan Kusini ilikuwa takriban 230.

Idadi hii mpya inaifanya idadi nzima ya watu waliokimbia Sudan Kusini tangu Julai Saba kuwa watu 5,015. Leo Dobbs ni msemaji wa UNHCR, Geneva.

(Sauti ya Leo Dobbs)

“Zaidi ya asilimia 90 ya wanaowasili upya ni wanawake na watoto chini ya miaka 18. UNHCR inatarajia watu wengi zaidi kukimbilia Uganda, hususan wakati huu ambapo vituo vya upekuzi vimeondolewa kwenye barabara ya Juba-Nimule inayounganisha mji mkuu wa Sudan Kusini na Uganda.”