Baraza Kuu laadhimisha Siku ya Mandela kwa mkutano maalum
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limekuwa na mkutano leo kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, ukihudhuriwa pia na nguli wa muziki aliye pia Balozi wa Amani katika Umoja wa Mataifa, Stevie Wonder.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Baraza Kuu, Mogens Lykketoft, amesema sasa ndio wakati mwafaka hata zaidi wa kushikia bango maadili aliyopazia sauti Mandela.
Amesema wakati huu ni mwafaka kwa sababu watu kote duniani wanaibuka kutoka kwenye uchungu wa mashambulizi ya kigaidi na mizozo, wahamiaji na wakimbizi wakifariki kwenye nchi kavu na majini, na umaskini na tofauti za kitabaka zinapoendelea kuwanyima watu haki zao za msingi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, amesema kujitoa kwa Mandela kulikuwa huduma siyo tu kwa watu wa taifa lake, lakini pia kwa watu kote ulimwenguni, kwa kuwapa matumaini ya kutimiza ndoto na matamanio yao.

Eliasson amesema, kiini cha Siku ya Mandela ni kufanya kazi ya kujitolea kwa watu na sayari dunia.
Ameongeza kuwa kauli mbiu ya siku hii ikiwa ni: “Chukua hatua, hamasisha mabadiliko” ina lengo la kuichagiza familia ya ubinadamu kufanya juhudi zaidi ili kujenga dunia yenye amani, endelevu na yenye usawa.
“Kuna mengi tunayoweza kufanya. Fundisha mtoto. Walishe wenye njaa. Safisha eneo au tunza mazingira yako. Jitolee kuhudumia hospitali au kituo cha jamii. Saidia familia ya wakimbizi. Kuwa sehemu ya vuguvugu la Mandela ili kuifanya dunia iwe mahali bora. Hakuna anayeweza kufanya kila kitu, lakini kila mtu anaweza kufanya kitu fulani.”