Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#UNCTAD14: Wakopeshaji wacheza kamari kuangaziwa

#UNCTAD14: Wakopeshaji wacheza kamari kuangaziwa

Mkutano wa 14 wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD ukianza leo mjini Nairobi, Kenya Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt. Mukhisa Kituyi amezitaka nchi zinazoendelea kuwa makini na wawekezaji wapya aliowafananisha na wacheza kamari.

Dkt. Kituyi amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Radio ya Umoja wa Mataifa kabla ya mkutano huo unaotarajiwa kufunguliwa na mwenyeji Rais Uhuru Kenyatta na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

(Sauti ya dkt. Kituyi)

Hivyo ametoa pendekezo ili kuepusha zahma kama iliyotokea huko Argentina ambako wawekezaji wa aina hiyo huondoa fedha zao bila kujali umma na kwenda kuwekeza kwenye faida zaidi.

(Sauti ya dkt. Kituyi)

Mkutano wa 14 wa hufanyika kila baada ya miaka minne ambapo lengo ni kupatia chombo hicho mamlaka mpya na hutanguliwa na majukwaa mbali mbali ikiwemo lile la bidhaa.

Katika jukwa la bidhaa lililohitimishwa Jumamosi, ripoti ya UNCTAD imebainisha kuwa nchi zinazotegemea kuuza nje bidhaa ili kujipatia fedha za kigeni hupoteza asilimia 67 ya mapato ya mabilioni ya dola ya biashara hiyo kutokana na ankara za biashara zinazoandikwa kidanganyifu.

Ripoti hiyo inatokana na utafiti wa miongo miwili kutoka Chile, Cote d'Ivoire, Nigeria, Afrika Kusini na Zambia ikiangazia bidhaa kama vile kakao, dhahabu, mafuta na shaba kutoka nchi hizo.

image
Kakao nchini Sao Tome na Principe. (Picha:Ifad/Susan Beccio)
Dkt. Kituyi akizungumzia ripoti hiyo amesema inadhihirisha jinsi udanganyifu kwenye ankara za biashara unavyochochea usafirishaji haramu wa fedha na kuathiri maendeleo ya nchi hizo zinazotegemea kipato kutokana na kuuza nje bidhaa zake.

Ripoti hiyo inaonyesha mwelekeo wa nyaraka zisizo sahihi kwa mauzo ya bidhaa za nje kuelekea nchi kama vile China, Ujerumani, Hong Kong(China), Italia, India, Japan, Uholanzi, Hispania na Marekani.