Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuibuka kwa machafuko Sudan Kusini kwazua hofu ya baa la njaa- FAO

Kuibuka kwa machafuko Sudan Kusini kwazua hofu ya baa la njaa- FAO

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), limeonya kuwa mamilioni ya watu wasio na uhakika wa kuwa na chakula nchini Sudan Kusini watalazimika kutumbukia kwenye baa la njaa, iwapo kuibuka machafuko mapia kutavuruga mchakato hafifu wa amani.

FAO imetoa wito kuwepo utulivu, na kuonya kuwa iwapo amani haitaimarishwa, gharama ya mapigano kwa binadamu itaongezeka kutokana na kuenea kwa njaa nchini Sudan Kusini.

Tathmini ya hivi karibuni mwezi uliopita, imeonyesha kuwa Sudan Kusini tayari ilikuwa katika hali tete, watu milioni 4.8 wakiwa hawana uhakika wa kupata chakula, huku viwango vya utapiamlo vikiwa juu.

Tathmini hiyo ilibashiri kuwa kutakuwepo uhaba mkubwa wa chakula katika miezi ijayo nchini Sudan Kusini, na kuonya kuhusu hatari ya baa la njaa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.