Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji kwa wasichana vigori Afrika Mashariki

Uwekezaji kwa wasichana vigori Afrika Mashariki

Juma hili tarehe 11, dunia imeadhimisha siku ya idadi ya watu.  Maudhui ya mwaka huu ni uwekezaji kwa wasichana vigori.

Shirika la Umoja wa Mataifa  la idadi ya watu UNFPA linasema licha ya hatua zilizopigwa katika usawa wa kijinsia, wasichana vigori bado wanasalia katika mazingira hatarishi kwani wengi hunyimwa haki, na kukatizwa ndoto zao kutokana na ubaguzi, unyanyasaji  na umasikini. Sehemu nyingine za dunia, msichana akishafikia hatua ya kuvunja ungo anatizamwa na jamii au familia yake kama ambaye yuko tayari kwa ndoa, ujauzito, na kujifungua.

Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA, Dr. Babatunde Osotimehin, anasema msichana huyo anaweza kuolewa na kulazimika kuacha shule huku akikumbana na magonjwa kama vile fistula kwa kuzaa kabla hajawa tayari  kimaumbile, na pia anaweza kunyimwa haki zake za kimsingi.

Anasema ikiwa haki za wasichana vigori zitatimizwa, wanaweza kustawisha dunia kwa namna kuu, wakithaminiwa na kusaidiwa wanakuwa na afya na wanaweza kuchomoza kutoka katika umasikini.