Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Zeid asikitishwa na shambulio la Nice, Ufaransa

Kamishna Zeid asikitishwa na shambulio la Nice, Ufaransa

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameelezwa kusikitishwa na mauaji ya raia jijini Nice, Ufaransa, katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa kwa kutumia lori kama silaha.

Katika taarifa iliyosomwa na msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu jijini Geneva, Uswisi, Kamishna Zeid amesema shambulio hilo ni pigo jingine la watu wenye itikadi kali linalolenga kiini cha ubinadamu.

Amesema dunia inakabiliwa na mashambulio mengi ya kikatili, akitaja mifano ya mshambulizi ya Baghdad, Brussels, Dhaka, Istanbul, Medina, na Orlando, akiongeza kuwa sasa ubinadamu unakabiliwa na dhana inayozalisha wakereketwa wa itikadi kali wanaofurahia kuua.

Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva

“Pale mbinu moja ya kuua inaposhindikana – mathalani kuteka ndege, kutega mabomu, na kutumia bunduki – wanapata mbinu nyingine. Jitihada zetu zinapaswa kupangwa kwa umakinifu na ustadi mkubwa. Haitoshi kuimarisha usalama. Tunapaswa kuvunja dhana yenyewe, hadi pale itakaporejeshwa inapopaswa kuwa- yaani isiwepo kabisa.”